Friday, August 31, 2012

KWA ELIMU HII TUTAFIKA? - Alexander Mtweve


Kama kuna kitu ambacho kinaweza kuonesha mwelekeo wa taifa lolote duniani kimaendeleo kwa miaka kadhaa ijayo, basi ni mfumo wake wa elimu.
Nchi nyingi ambazo kwa sasa zinafurahia maendeleo ya kiuchumi na kiviwanda n
i matokeo ya uwekezaji mzuri uliofanyika hapo awali katika elimu, na suala linakuja siyo tu elimu, bali elimu bora ikiwa na mfumo unaochochea ukuzaji wa vipaji na uwezo wa wanafunzi.
Kwa upande wa nchi nyingi za kiafrika ambazo zimerithi mfumo wa elimu kutoka kwa watawala wetu wa kikoloni, suala la kuwa na mfumo mzuri wa elimu bado ni ndoto, kwani mfumo uliopo umewekezwa kwenye itikadi ileile ya kuwalisha watoto matango pori.
Ninachokimaanisha hapa ni kuwa, mwanzoni wakoloni waliwapa elimu waafrika wachache ili waweze kuwasaidia katika shughuli zao za kiutawala na kuendesha uchumi wa kikoloni, cha ajabu ni kuwa hata baada ya kupata uhuru nchi nyingi za kiafrika zimesalia kuutegemea mfumo ambao muda wake umekwisha.
Siyo kitu cha ajabu kumsikia mzazi akimwambia mwanae “soma kwa bidii mwanangu ili uje kupata ajira nzuri utusaidie sisi wazazi wako”. Jambo hili linajengeka kichwani mwa mtoto na kuona kuwa njia pekee ya kupata ajira/maisha mazuri ni kusoma kwa bidii. Sisemi kuwa kusoma kwa bidii ni kitu kibaya, ila unajua mwanao anasoma nini?
Nakumbuka wakati ninsoma shule ya msingi kulikuwa na masomo mengi ambayo mwisho wa siku huunganishwa kwenye mitihani mitatu (Hisabati, Maarifa na Lugha). Katika masomo haya kila mtu alikuwa na kiwango cha aina yake cha ufaulu, kila mmoja alikuwa na uwezo tofauti kulingana na somo.
Kwa upande wangu lugha ndilo lilikuwa somo nililoliweza zaidi, japo katika masomo mengine pia nilifaulu vizuri na kufanikiwa kujiunga sekondari. Huku sasa nikajikuta niko katika dunia nyingine tofauti kabisa!
Ile staili ya kufundishwa ya shule ya msingi ikawa ni kama imegeuzwa juu chini. Mchakamchaka wa kufundishwa ambao sikuuzoea shule ya msingi nikakutana nao sekondari na hakuna njia nyingine isipokuwa kuendana na mazingira.
Ile habari ya kupata hesabu 45 kati ya 50 haikuwepo tena! Maswali ya nchi gani inaongoza duniani kwa uzalishaji wa motokaa (enzi hizo tuliambiwa ni Ujerumani, japo kwa sasa najua ni Japani isijekuwa wanafundishwa ni Ujerumani bado!) sekondari haikuwepo tena.
Kwa kifupi mambo yalikuwa yamebadilika mno, isipokuwa kitu kimoja tu: “fundisha ya bora liende” au “ndivyo mtaala unavyosema”. Katika hili kwa kweli sina sababu ya kuwalaumu walimu, kwani wao wanafundisha kulingana na mtaala wa elimu unavyosema, japo walimu wachache wajanja walitupenyezea ujuzi wao wa ziada juu ya mambo muhimu nje ya mtaala.
Kwa jinsi mabo yalivyokuwa yakienda nikapata wasiwasi kama kile ninachokitarajia (maisha mazuri) nitakipata kweli. Ukweli ni kwamba sikuwa na malengo maalumu juu ya nini hasa ninataka kuja kukifanya maishani ili kujisikia kwamba nina maisha mazuri. Kuna wakati nilikuwa na ndoto ya kuwa rubani, raisi, mbunge, mfanyabiashara na kila aina ya ndoto.
Sikuwahi katika kipindi hicho kujua ni kwa jinsi gani ninaweza kuunganisha kusoma kwa bidii nilikoambiwa na kupata ajira na maisha mazuri. Nilisikia rafiki zangu wakilalamika (hasa wanaopenda sayansi) kuwa hawakuwa wakisoma sayansi, bali historia ya sayansi. Japo sikuelewa kiundani sana, ila nilijua matarajio yao hayakufikiwa.
Vitabu vilivyokuwa vikitumika kufundishia masomo ya sayansi ni vya zamani kiasi cha wanafunzi kuwa na wasiwasi kuwa mambo mengine wanayofundishwa huenda yamepitwa na wakati na hayatumiki tena katika ulimwengu wa kiteknolojia. Nafikiri pia ilichangia wanafunzi wengi kujikuta wakiangukia katika masomo ya sanaa hata kama walipenda kuwa wanasayansi.
Turudi kwenye mada yetu. Kwa muda mfupi tulishuhudia mabadiliko katika wizara ya elimu ambapo ilikuwa ni kama kila waziri akiamka anakuja na fikra zake na kuzifanya sera ya elimu. Nakumbuka Mungai aliwahi kuunganisha masomo (eti Fizikia na Kemia kama somo moja) akafuta somo la kilimo na masomo ya biashara ambayo angalau yalikuwa na mwelekeo wa moja kwa moja juu ya kitu mtu anataka kukifanya maishani mwake.
Kikubwa ni kwamba elimu ilikuwa haimsaidii mtu kufikia malengo yake, ila tu ilikuwa inakupeleka ngazi nyingine ya juu zaidi ya kielimu. Ukweli ni kuwa wengi tulikuwa tunasoma ili tufaulu mitihani ya mwisho na kwenda ngazi ya juu kielimu kama kidato cha tano na cha sita na hatimaye chuo kikuu.
Kwa kuwa akili za wanafunzi wengi zimewekezwa kwenye kufaulu, basi mtu akishindwa kufaulu mtihani anaona kama dunia imegeuka juu chini. Na wengi wakifeli mitihani huona kama maisha yao yamefika mwisho kwa kuwa njia pekee aliyoambiwa ya kufikia mafanikio ni kusoma kwa bidii, sasa amekata tamaa kwani pamoja na kusoma kwa bidii amefeli mitihani.
Kutokana na msukumo mkubwa kuwekwa kwenye ufaulu, wanafunzi wengi hujikuta wakiweka mkazo zaidi kutaka kufaulu mitihani. Hii hupelekea hata wazazi kuwaona watoto wao kuwa hawana akili ikiwa watashindwa kufaulu mitihani ya taifa.
Cha msingi cha kujiuliza hapa ni kuwa, kwa mfano amesoma miaka saba shule ya msingi, na mtihani anaufanya mara moja, huenda siku hiyo hali yake kisaikolojia haikuwa nzuri na akajikuta ameshindwa kufanya vizuri, je inamaanisha kuwa alikuwa hajiwezi kimasomo? Kwa nini usiwepo mfumo mbadala wa kupima uwezo wake na wa kumpeleka mbele?
Matokeo ya kuwekeza sana kwenye ufaulu badala ya uelewa hupelekea wanafunzi na wazazi wao pamoja na walimu kujihusisha na udanganyifu katika mitihani, kwani wanajua ya kuwa kufaulu mtihani wa taifa ndiyo njia pekee ya kufanikisha maisha yao. Unakuta mtoto kafaulu kwenda sekondari lakini hata jina lake hawezi!
Ni ukweli usiopingika kuwa mfumo wetu wa elimu umejiwekeza sana katika nadharia na kukariri na kumnyima mwanafunzi kujenga na kukuza uwezo wake hivyo kumlazimisha mwanafunzi kusoma vitu vingi na kupunguza uwezo wake katika masomo anayoyamudu zaidi.
Ni vema kumuendeleza mtoto kulingana na kipaji chake ili aweze kuonyesha uwezo wake zaidi na kupata matunda mengi zaidi kutoka katika kipaji chake. Huenda siku zote tunajiuliza inakuwaje tunao wasomi wengi lakini mbona hatuna maendeleo na bado tunaagiza wasomi kutoka nje kwa ajili ya shughuli mbalimbali nchini.
Sababu kubwa ni kwamba elimu yetu inaua vipaji badala ya kuvikuza na hivyo tunajikuta tukipoteza wataalamu wengi kupitia mfumo duni wa elimu unaowalazimisha wanafunzi kukariri vitu visivyo na umuhimu ili waweze kufaulu tu, huku tukisahau jambo la msingi zaidi ambalo ni kuwa na watu mahiri katika jambo fulani.
Tukitaka kwenda mbele, ni muhimu kuwekeza vizuri katika elimu yetu kama ambavyo mataifa mengine yaliyoendelea na yale yanayoendelea kwa kasi yalivyofanya. Hata katika baadhi ya nchi majirani tunaweza kujifunza.
Mfumo wetu wa elimu ukiwa vizuri, wazazi wataacha kuwakimbizia watoto wao shule za kiingereza na zile za St. Nanihii kwa kudhani kuwa ndiko kuna elimu bora zaidi (kwa upande fulani ni kweli) na kuwaacha kina Kayumba wakibaki bila kimbilio.

Tuesday, August 21, 2012

TUSIHARIBU SENSA KWA MITAZAMO YA DINI ZETU, TUSHIKAMANE KAMA WATANZANIA - Samora Julius


Kwanza kabisa ningependa kutoa wito wangu kwa watanzania kushiriki kwa ustadi na umakini wa hali ya juu katika zoezi zito na muhimu katika taifa letu ambalo si lingine bali ni sensa.

Ndugu watanzania, hakuna kitu muhimu kama kushiriki katika shughuli ya kupanga maendeleo yetu wenyewe, kushiriki katika sensa ni kuonyesha uzalendo wako katika taifa lako. swala la sensa si Tanzania tu ni bali ni swala la NCHI ZOTE na umuhimu wako hujikita katika mambo makuu kama matatu hivi nayo ni:

(1) kuangalia hali ya uchumi na ustawi wake wa jamii.
(2) kutayarisha mipango ya maendeleo.
(3)kuweka misingi itakayosaidia kufanya maamuzi.

Ndugu watanzania, kuna mawazo machafu yanayoenezwa na watu au kikundi cha watu kuwaada watanzania kutoshiriki katika zoezi la sensa hapa napata HOFU tena kubwa kwa mtanzania huyu anafanya hivyo kwa manufaa ya nani na kwalengo gani?

Tukianza kujitambua kwa DINI zetu katika zoezi hili la sensa basi tunapotaka kuelekea ni pabaya sana maana tukitoka kwenye kutambuana kwenye DINI tutaamia kwenye madhehebu yetu kwamba hawa ni wengi kuliko wale,tukishamaliza kwenye DINI tutahamia kwenye makabila yetu. Ndugu zangu tuwe makini JUU YA JAMBO HILI LA SENSA NA DHANA YA UDINI.

Tukumbuke sisi ni watanzania na tutabaki kuwa watanzania bila kujali makabila wala dini zetu, swala la sensa lisije likawa kama chanzo cha kuvuruga amani tulionayo maana kuna watu wachache wanaotaka kutuvuluga watanzania katika mambo muhimu katika maendeleo yetu.

Ifahamike kwamba SENSA ni kama moja wapo ya nyenzo muhimu katika kupanga na kujitasmini sisi kama watanzania wapi tumetoka na wapi tunapotaka kuelekea si kwa manufaa ya watu au kikundi cha watu wachache na bila kuangalia DINI zao au makabila au sehemu wanazotoka.

WITO WANGU KAMA MTANZANIA NISIYEJITAMBULISHA AU KUJIPAMBANUA KWA KABILA au DINI YANGU NAPENDA KUWASIHI WATANZANIA KUSHIRIKI KWA MOYO MMOJA KATIKA ZOEZI LILILOPO MBELE YETU KWA KUJITAZAMA KAMA MTANZANIA NA SI VINGINEVYO.

MUNGU IBARIKI TANZANIA,MUNGU IBARIKI AFRIKA

JENGO LA KANISA TAG CITY HARVEST LAWEKWA WAKFU RASMI

HATIMAYE jengo Kanisa la TAG City Harvest limezinduliwa na kuwekwa wakfu na Askofu Mkuu wa Tanzania Assemblies of God, Rev. Dk. Barnabas Mt...