Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na
mfululizo wa matukio yanayoashiria
uvunjifu wa amani, umoja na utengamano wa
taifa letu la Tanzania, haya
ndiyo yanayonisukuma kutoa tamko hili leo
ili kuonya na kushauri.
Katika siku za karibu kiumeibuka makundi
mbalimbali ya kidini ambayo
yalianza kutoa matamko yenye kuchochea
ghasia za kidini Tanzania, na
pengine kauli hizo ndizo zinazotimizwa kwa
vitendo hivi sasa.
Miongoni mwa matukio hayo ni:
Januari sita mwaka huu, kikundi kimoja
kinachoitwa JUAKATA, kiliitisha
kongamano la kujadili katiba mpya
Tanzania, kwa upande wa Waislam.
Katika kongamano hilo lililofanyika kwenye
Ukumbi wa Diamond Jubilee,
Dar es Salaam kauli zifuatazo:
1. Lazima Rais ajaye atoke Zanzibar
2. Kukabiliana na ukuaji wa kasi wa dini
ya Kikristo
3. Kupinga Muungano ili kuupa nguvu
Uislamu
4. Kupigana kufa na kupona kutetea maslahi
yao wakati huu wa kuandaa
katiba mpya.
Kauli hizo zilitolewa na Sheikh Nasor
Mohameed, kutoka Zanzibar,
ambaye alikuwa mgeni rasmi. Baadaye
zikaandaliwa kanda za CD
zilizosambaza ujumbe huo.
Uchunguzi unaonesha kuwa miongoni mwa
makanisa yaliyochomwa hivi
karibuni huko Zanzibar ni ya EAGT, Elimu
Pentecost na TAG, Anglikana,
Katoliki na FPCT, hivyo kujenga taswira ya
ubaguzi wa kidini ambao
kama hautapatiwa dawa unaweza kuligawa
taifa la Tanzania kama
ilivyotokea Nigeria na kwingineko barani
Afrika.
Hofu yangu ni kuwa, roho hii ya ubaguzi wa
kidini ambayo Baba wa Taifa
hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere
aliifananisha na dhambi ya kula
nyama ya mtu, imekuwa ikiyatafuna mataifa
ya Afrika kama ifuatavyo:
1. Mwaka 2000, vuguvugu la kuanzishwa kwa
utawala wa Kiislamu
(Sharia), lilianza kwenye majimbo ya
Kaskazini mwa Nigeria, miaka
michache baadaye majimbo kadhaa
yakajitangazia sheria hizo na tangu
wakati huo kumekuwa na mapambano
yasiyoisha. Takwimu zinaonesha kuwa
katika miaka ya karibuni zaidi ya Wakristo
500 wameuawa kikatili na
makanisa kuchomwa moto.
2. Roho hii imekuwa ikienea kwa kasi
katika maeneo mbali mbali ya
Afrika ambapo imelikumba taifa la Mali,
majimbo ya kaskazini tayari
yametangaza kujitenga na kuna vuguvugu
lenye kuhusisha mapigano ya
silaha.
3. Itakumbukwa kuwa wiki chache tu
zilizopita vuguvugu hili la kudai
utawala wa kidini liliibuka nchini Kenya
ambapo watu wanaojiita
wanaharakati walianzisha madai ya kutaka
eneo la Pwani kujitenga na
Jamhuri ya Kenya na kujitangazia taifa la
Kiislamu.
4. Ni wakati huu ambao kundi la Uamsho
linalopinga kuandikwa kwa
katiba mpya kabla ya kuitishwa kwa kura ya
maoni ili wanzazibar waamue
kuhusu Muungano liliibuka na kuanzisha
ghasia Zanzibar ambazo
zimepelekea makanisa kadhaa kuchomwa moto
na mali kuharibiwa, huku
watu wa bara wakitishiwa maisha.
USHAURI WANGU KWA SERIKALI NA VIONGOZI WA
DINI
Ni wajibu wa kila Mtanzania kutii sheria
na mamlaka kwa kuwa zimewekwa/
kuruhusiwa na Mungu, hivyo kuziasi ni
Kumuasi Mungu, yaani ni dhambi.
Hivyo kila Mtanzania anastahili kukumbuka
wajibu wake wa kutii
mamlaka.
Viongozi wenzangu wa dini wakumbuke kuwa
wana wajibu mkubwa katika
jamii, na jamii inawasikiliza hivyo ni
vyema wakawa makini katika
matamshi na maelekezo yao ili wasiwe
chanzo cha kuchochea vurugu za
kidini na uvunjaji wa amani.
Ni vyema wakati huu wa kuandikwa kwa
katiba mpya, kila kikundi
kikafuata utaratibu uliowekwa badala ya
kuchochea ghasia ambazo
madhara yake yatawakumba watanzania wote
ikiwa ni pamoja na wao
wenyewe watoto na wajukuu zao.
Pia ningependa kuwashauri viongozi wa
serikali kusimama imara katika
kusimamia sheria na haki, na kuepuka kauli
au vitendo vitakavyofanya
baadhi ya watanzania kudhani kuwa
hawatendewi haki.
Ni vema ieleweke kuwa matukio kama haya ya
uvunjaji wa amani
yasipodhibitiwa na kukomeshwa haraka
yanaweza kuumba chuki ambayo
inaweza kuibua mlipuko mkubwa na machungu
kwa wananchi na matokeo yake
yakawa mabaya kwa Taifa zima. Hekima na
busara inatufundisha kuwa
tusipoziba ufa tutajenga ukuta.
Ni vyema wenye dhamana ya kuongoza
wakakumbuka kuwa wanawajibu mbele
ya Mungu aliyewaweka au kuwaruhusu kuingia
madarakani na siku moja
watatoa hesabu mbele zake.
Mwisho, natoa wito kwa watanzania wenzangu
tuulinde umoja, amani na
utengamano wa taifa letu, tuikimbie dhambi
ya ubaguzi kwa kuwa
tukiiruhusu itatuangamiza sote. Tuliombee
taifa letu na kukiwa na
mbegu ya chuki tuimalize kwa njia ya
majadiliano na vikao vya pamoja
vinavyohusisha viongozi wa dini zote na
serikali pia.
Imetolewa leo 28/05/2012
Na Dk. Barnabas Mtokambali
Askofu
Mkuu wa TAG