Monday, October 17, 2011

UWAJIBIKAJI KATIKA KUPATA HAKI - by Azgard Stephen

Ninamshukuru Mungu tena kwa kunipa nafasi hii ya kukuletea waraka ama makala hii muhimu sana katika maisha yako kwa ujumla. Nasema hivyo kwani usipotambua haki yako na wajibu ulio nao kwako mwenyewe, kwa jamii na kwa Mungu unayemtumikia; kuna mambo kadhaa yatakwenda ndivyo sivyo halafu utabaki kusema kwa nini Mungu hajibu maombi yangu, kwa nini serikali hainitendei haki, kwa nini niko hivi n.k.
UTANGULIZI
Wajibu: ni ile hali ya kuhusika na utendekaji wa jambo fulani.
Responsibility is having the duty of looking after someone, something, so that one can be blamed if things go wrong.
Haki: ni faida anazopata ama kile anchopaswa kufanyiwa ama kupata mtu
Rights are the political, sociala and other advantages to which someone has a just claim, morally or legally.
Nimetamani sana kulizungumzia jambo hili kwa sababu kuu mbili. Moja, kuna watu wanapenda sana kudai haki na wako mstari wa mbele kweli, lakini hawataki kuwajibika; yaani inapofikia wakati wa kuwajibika wao wako mstari wa nyuma. Mbili, kuna watu wanawajibika sana , lakini kwa kutokujua kuwa ipo haki kwa ajili ya uwajibikaji wao, wamepoteza haki zao. Kwa hiyo naweka somo hili ili wale wanaopenda kudai haki bila kuwajibika wabadili mtazamo, na wale ambao wanawajibika bila kudai haki zao wajue kwamba wanapaswa kudai haki zao.
Nilipofundisha somo la mafanikio nilisema kwamba, hakuna mafanikio bila mafanikio; hapa ninasema hakuna haki bila wajibu. Sina nia ya kukuweka chini ya sheria sana , ila ninataka nikupe misingi ya kuishi maisha ya uhakika na ushindi kila siku. "A responsibble man always gets succeed" Kibiblia, kila aliyewajibika alipokea.
Sasa naomba tutazame vifungu kadha wa kadha vya Biblia ili viweze kukusaidia kuelewa jambo hili kibiblia maana unaweza kusema sasa nimeanza kuzungumza siasa. Mimi sio mwanasiasa na sina mpango wa kuwa mwanasiasa; ila sio dhambi kuwa mwanasiasa.
Matendo Ya Mitume 10:1-8
Hapa tunamuona Kornelio, akida wa kikosi cha kirumi, maana yake ni kwamba hakuwa myahudi. Huyu ndugu alisikia habari za Mungu wa wayahudi, na Yesu Kristo mwana wake; akavutiwa naye. Akaanza kumtafuta kwa nguvu zote, kwa maombi na sadaka. Katika mstari wa 4, malaika akatumwa na Mungu kwa Kornelio na kumwambia,"...sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu" Kile malaika anachosema maana yake ni kwamba, "uwajibikaji wako kwa njia ya maombi na sadaka umeonekana mbele za Bwana." Ukifanikiwa kuendelea mstari wa 9 hadi mwisho wa sura hii utaona kwamba huyu ndugu alipata wokovu (haki). Kumbuka kwamba huyu ndugu alikuwa anatoa sadaka na maombi, sasa kilichokuwa katika maombi yake ndicho Mungu alicholeta. Kumbuka sana kuwa huyu alikuwa mrumi, anamtaka Mungu wa wayahudi. Na ndio maana sehemu nyingine Biblia inasema, "...mkinitafuta kwa bidii mtaniona." Tena sehemu nyingine Yesu anasema, "...mkinitumikia (mkiwajibika), baba yangu aliye mbinguni atawaheshimu (haki)."
Yohana 1:12
"Na wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu..."
Maana yake ni kwamba, ili kufanyika mtoto wa Mungu (kupata haki ya kuwa mwana) ni lazima kwanza kumpokea Kristo (kuwajibika). Sasa unaweza kuniuliza kwa nini ninasema kumpokea Kristo ni kuwajibika, jiulize tu kwa nini Yesu aliwaambia wanafunzi wake wabebe misalaba yao wamfuate. Kwa hiyo unapowajibika kumbeba mwana ndipo unapata neema ya kufanyika mwana wa Mungu. Sasa nizungumze kidogo juu ya mwana. Ukiwa mtoto una haki za msingi kwa baba,kule kwa wenzetu wazungu, baba asipomtimizia mtoto haki zake, serikali inaweza kumfunga jela! Kuna vitu vingine huwezi kuchukua isipokuwa wewe ni mtoto. Hata urithi anapewa mwana, hivyo hata ufalme wa Mungu huwezi kurithi, yaani huna haki ya kuurithi isipokuwa umefanyika mwana. Hivyo Biblia inaposema sisi tukimpokea Kristo tunafanyika wana wa Mungu maana yake ni kwamba tunakuwa na haki ya kwenda kwa baba kama watoto na kudai haki zetu za msingi. Lakini pia uelewe kwamba, kwa mfano; si lazima mtoto amwambie baba nataka kwenda shule, ila ni wajibu wa baba kuangalia kama umri wa mtoto kwenda shule umefika ampeleke. Na ndio maana kuna vitu vingine hatumwombi Mungu lakini unashangaa umepata! Unaweza ukajiuliza, mbona hili hata sijaomba lakini nimepokea? Ni kwa sababu wewe ni mtoto, kuna haki zako nyingine huzijui lakini Baba wa mbinguni anajua; anakufungulia 'Junior Jumbo account', bima ya afya, bima ya maisha n.k. Hiyo ni kazi ya baba. Lakini sasa sikwambii usiombe, kwani si kila wakati baba atakuletea zawadi, saa nyingine lazima "...ulete hoja zenye nguvu..." kwa baba ndipo akupe hicho unachoomba.
Isaya 38:1-8
Hapa tunaona Isaya nabii anatumwa na Mungu kumpelekea Hezekia mfalme ujumbe kwamba atengeneze mambo ya nyumba yake kwani siku zake za kufa zimefika. Hezekia akamgeukia Bwana na kuomba, angalia mstari wa tatu, "...ee Bwana, kumbuka haya nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako..."
Hezekia alikuwa anamkumbusha Mungu jinsi alivyowajibika ili apewe haki ya kuendelea kuishi. Biblia inasema katika mst 5, "...mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama nimeziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano." naamini umeona hili, baada ya Hezekia kumkumbusha Mungu juu ya namna alivyowajibika, ndipo hapo Mungu anatoa haki ya kuishi miaka 15.
Angalia jambo hili, kinachompa muda zaidi Hezekia ni kuwajibika katika ufalme wake, lakini pia kuwajibika kumkumbusha Mungu juu ya uwajibikaji wake. Na ndio maana hapo awali nilisema, kuna watu wanawajibika sana lakini kwa kutowajibika kukumbusha ama kudai haki zao, wamezikosa.
2Nyakati1:1-13
Katika eneo hili, Sulemani anatawazwa kuwa mfalme wa Israel baada ya baba yake mzee Daudi. Biblia inasema, Sulemani akapanda hadi Gibeoni, akamtolea Mungu ...sadaka elfu za kuteketezwa juu yake. Mara usiku ule Mungu akamtokea Sulemani na kumwambia, "...omba lolote utakalo nikupe." Sulemani akaomba hekima na maarifa ili aweze kuwaongoza watu wa Mungu. Mungu akampa pamoja na mali .
Ninachotaka uone hapa ni kwamba, Sulemani alimtolea Mungu sadaka (aliwajibika) lakini hakuomba chochote sambamba na sadaka hiyo. Biblia haisemi alitoa zaka, maana zaka ni kwa ajili ya Bwana mwenyewe, huna ushirika nayo, lakini inasema alitoa sadaka. Hivyo Mungu alitegemea kusikia Sulemani anataka nini sambamba na sadaka hiyo, Sulemani akakaa kimya. Mungu akaamua kushuka na kuuliza. Ndipo Sulemani akatoa haja ya moyo wake. Lakini pia anaomba kitu ambacho ni kwa aajili ya kutimiza wajibu ule ule wa Mungu, Mungu akampa na mali . Nataka uone kwamba, uwajibikaji wa Sulemani katika kutoa sadaka ndio uliompa haki ya kupewa hekima, maarifa na mali . Si kwamba hapo awli hakuwa na hekima wala maarifa, ila hekima na maarifa aliyokuwa nayo vilikuwa vinamtosha kujiongoza mwenyewe, lakini sasa lipo kundi la Mungu kubwa; akipima kiwango cha hekima na maarifa aliyo nayo havitoshi kuongoza, hivyo alipopata hii nafasi, alipeleka hoja hiyo ya msingi kwa Bwana. Bwana akampa na mali.
Ukifuatilia kwa makini maisha ya Ibrahimu, utagundua kwamba, alipotoa Mungu alimpa, na kila Mungu alipompa alitoa. Maana yake ni kwamba, alipowajibika Mungu alimpa haki; lakini pia alipopokea haki (ambayo hakuiwajibikia) aliwajibika.
Mwanzo 18:1-15
Hapa tunaona Bwana pamoja na malaika wawili walikuwa wanapita kuelekea Sodoma na Gomora kuangamiza hii miji. Ibrahimu anawakaribisha na kuwaandalia chakula. Walipokula walimuuliza kwa habari za Sara. Wakamwambia katika mstari wa 10, "...tazama nitakurudia wakati uu huu mwakani, na Sara mkeo atapata mwana wa kiume..."
Kilichomfanya Bwana kutoa ahadi hii ni ukarimu (uwajibikaji) wa Ibrahimu. Unaweza kuniuliza, kwani si Mungu alishatoa hii ahadi miaka 19 iliyopita? Jibu ni kwamba, kwa nini asijibu miaka kumi iliyopita ajibu leo, ama kwa nini asijibu miaka kumi ijayo? Tena zaidi ya hapo Bwana akaamua kubaki na Ibrahimu na kumueleza kile alichokusudia kufanya kwa ajili ya Sodoma na Gomora, kwa nafasi hii Ibrahimu akamuokoa nduguye Lutu. Kwa ufupi, Mungu aliona uwajibikaji wa Ibrahimu (kuandaa chakula) akampa haki (mtoto pamoja na kumtoa Lutu katika Sodoma).
Warumi5:1-11
Paulo mtume anajaribu kutueleza juu ya haki kwa njia ya imani. Paulo anasema, ...tumekwisha kuhesabiwa haki kwa njia ya imani. Lakini haishii hapo, anazungumzia maana ya kifo cha Yesu msalabani. Anaeleza kuwa ni upendo wa Mungu kwetu. Lakini swali la kujiuliza ni kwamba; kwani mtu akikupenda lazima afe kwa ajili yako? Inaleta mantiki? Maana leo tunaambiana 'nakupenda'; lakini je, umeshawahi kufa kwa ajili ya unayempenda? Maana utakufa mara nyingi sana kama kila unayempenda unakufa kwanza kwa ajili yake, tena kwa mateso makali mno! Lakini sasa Paulo anasema katika mstari wa 8 na 9, "Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye."
Tazama hiki kitu anazungumza, ...Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi... maana yake ni kwamba, hatukugharamia wokovu hata kidogo, tumepewa bure! Maana yake ni kwamba, kimsingi hatukupaswa kupewa maana hatukuwajibika hata kidogo. Lakini sasa angalia, ...zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake... Kumbe Yesu hakufa kwa sababu ya upendo tu, ila damu yake ituhesabie haki, yaani tukienda mbele za Mungu kudai haki ya wokovu, uponyaji n.k, Mungu akitazama wapi tumewajibika; damu ya Yesu inasimama na kusema, 'niliwajibika kwa ajili yao !'
Zamani za agano la kale, kila aliyesogea mbele za Bwana ilimpasa kwenda na sadaka ya kuteketezwa ili kumwaga damu. Hizo damu ziliwahesabia haki, yaani zilionesha uwajibikaji wao. Maana yake ni kwamba, kwa yule asiyekuwa na kitu cha kusogeza kwa Bwana hakuweza kuuona uso Bwana. Leo, badala ya kupokea wokovu kwa kutoa damu ya mnyama, ng'ombe, kondoo, njiwa n.k damu ya Yesu ipo! (Sikwambii usitoe sadaka.)
Kwa hiyo, damu ya Yesu inaonesha uwajibikaji wetu mbele za Bwana, na ndio maana popote pale unaweza kuutafuta uso wa Bwana, iwe chooni, barabarani, ndani ya basi, popote! Ukiutafuta tu uso wa Bwana, damu ya Yesu inajenga madhabahu mbinguni, Mungu anakusikiliza; Haleluya!!
Kwa ufupi tu kabisa niseme, Yesu aliwajibika kwa ajili yetu na ndio maana tunayo haki ya kusogea mbele za Bwana. Alipokufa msalabani alisema ...imekwisha... Tokea hapo tukawa huru kwenda kwa Bwana, saa yoyote, wakati wowote. Sasa naamini unanielewa kwamba, hatukupewa wokovu bure kama tunavyofikiri, ila Yesu alilipa!
Wagaratia 6:7
"Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; maana chochote apandacho mtu ndicho atakachovuna."
Kwa lugha ya hisabati (Mathematical language) hata 0 (zero) ni kitu. Maana huyu ndugu anasema ...chochote... yaani haijalishi ni nini. Kwa maana hiyo ukipanda hakuna utavuna hakuna, ama ukipanda 0 utavuna 0. Ukipanda 1 utavuna kadhaa (maana ukipanda tunategemea ulichopanda kizae zaidi ya ile mbegu. Lakini sufuri haizai).
Lakini ninachotaka tu uone hapa ni 'logic' iliyopo katika hii sentensi, "ukipanda...utavuna..." kwa maneno mengine, "usipopanda...huvuni..." Kwa lugha ngumu kidogo hapa Paulo anasema, 'Ukiwajibika...utapata haki" Fikiri kwa habari ya mkulima aliyepanda mbegu halafu akakosa mavuno, utaona jinsi anavyolalamika. Kitu anacholalamikia ni 'haki yake', maana amewajibika lakini hakupokea haki! Lakini pia ukimsikia mtu aliyepanda gunia moja la mahindi na kuvuna gunia moja akilalamika unaweza ukamshangaa, pengine na kumuuliza kwamba, unacholalamika ni nini wakati umevuna ulichopanda; lakini nikueleze kwamba huyu mkulima hakuvuna, mavuno ni kile unachopata nje ya mbegu, asikiaye na afahamu!
Naamini mifano hiyo inaweza kukuonesha uhusiano uliopo kati ya haki na wajibu. ipo mifano mingi sana katika Biblia inayozungumzia jambo hili, ikipata muda mwenyewe kasome habari za Hana, Esta, Daniel n.k. Nia yangu ni kukuonesha jinsi gani Biblia inautazama uwajibikaji wako.
Saa nyingine unaweza kujiuliza kwa nini Mungu hajibu maombi yako, lakini angalia kwanza, je umewajibikaje katika nafasi uliyopewa? Maana Biblia inasema sisi ni viungo vya Kristo, yaani kuna wengine ni macho, wengine ni masikio, wengine ni miguu, wengine ni meno, ulimi n.k. Sasa hakuna kiungo kisicho na kazi. Hivyo wewe kama kiungo cha Kristo timiza wajibu wako, kama ni mguu tembea, kama ni jicho ona, kama ni sikio sikia, kama ni jino tafuna, kama ni ulimi onja! Sasa wewe hujatimiza wajibu, yaani hujafanya kazi halafu unataka ule, kwa namna gani? Unapowajibika ndipo umuhimu wako unatambulika. Kuna msemo wa kiswahili unaosema, "Ng'ombe haoni umuhimu wa mkia wake mpaka siku umekatika."
Kwa kweli Mungu anapotuangalia saa nyingine anasikitika, maana wengine tumeokoka halafu eti tunasubiri kwenda mbinguni, hatufanyi kazi yoyote, tukidai eti hizo ni kazi za wachungaji, wainjilisti, akina Azgard, n.k. Sawa, lakini saa yaja ambapo, labda heshima yako imeshuka katika jamii, hata pale darasani unaposoma ukisimama na kuwaambia waache kelele ndio kwanza wanazidisha kelele; halafu unamrudia Mungu na kudai heshima, eti Mungu naomba uniheshimu mwenyewe. Mungu atajibu hayo maombi ipasavyo, "hizo heshima ni za wachungaji, wainjilisti, akina Azgard..." Ukiuliza kwa nini? Atakujibu, "Kwa sababu, ukinitumikia, Baba yangu aliye mbinguni atakuheshimu." Sasa wewe hujatumika halafu unataka heshima; ipi?
Nikuhamasishe tu kwamba, kila mmoja anayo karama aliyopewa na Mungu, tena Biblia inaiita kito cha thamani, maana yake ukiitumia katika kumtumikia utakula matunda yake. Hivyo kama unakaa ukisubiri kwenda mbinguni, hata kufagia ukumbi wa kanisa huwezi; kaa subiri, lakini mbinguni sio Marekani! Kazi ya karama ni kulijenga kanisa duniani, sio mbinguni!
Mimi siamini kwamba huna kitu cha kufanya kwa Bwana; unacho, hujajua tu unatakiwa kufanya nini. Nikushauri kwamba tafuta Mungu ameweka nini ndani yako halafu fanyia kazi uone kama Bwana hajaonekana kwako. Tatizo ni kwamba tumekuwa wavivu mpaka wa kutafuta vipawa ambavyo Mungu ameweka ndani yetu, hiyo ni hatari. wala huhitaji kwenda kwa nabii akuambie Mungu ameweka nini ndani yako, ila kaa na Bwana, muulize Bwana, halafu jaribu kila ambacho unajisikia kufanya kwa ajili ya Bwana. Kuna eneo utafika kila unachofanya unafanikiwa, kazi yako inakubalika; yaani unaona matunda ya ulichofanya. Ng'ang'ania hapo, muombe Mungu akuwezeshe. Utaanza kuona ufanisi ambao hujauona mwanzo.
Nikuulize, kama hujui kazi uliyoitiwa, ni lini hata ulikaa saa moja kuombea watumishi, uchumi wa nchi, viongozi wa nchi, nchi nyingine, jamaa yako? Maana tunafikiri kumtumikia Mungu ni kuhubiri tu, hata kuomba ni utumishi.
Mwaka fulani nilipanga kuomba kwa ajili ya nchi zaidi ya 100 duniani, yaani, kwa baadhi ya siku za mwaka nichukue kama nusu saa hivi kila siku kuombea nchi moja. Ule mwaka uliisha sikufikia hata nchi 50. Nikamuuliza Mungu kwa nini nilipanga jambo hili jema kabisa na nikashindwa kulitimiza? Roho Mtakatifu akanijibu, "hata huo ni utumishi." Maana yake, kama hujaitwa katika hilo eneo ni vigumu sana kutekeleza, maana hiyo ni taasisi iliyokamilika, ina watendaji katika ulimwengu wa roho, ina jeshi n.k. Ninachotaka uelewe ni kwamba, kama huoni cha kufanya, kwa nini usijaribu na jambo hili? Unaweza ukakaa kwenye hiyo Wizara ya maombi ukajikuta wewe ndio mwamuzi wa mambo yote yanayofanyika Tanzania , ama Afrika Mashariki, Ama Afrika."
Siku moja nikiwa njiani kutoka Dar, maeneo ya Korogwe, Roho mtakatifu akapitisha picha ya ajali mbele yetu, kama mita 200 hivi. nikampa taarifa mwenzangu niliyekuwa naye aombe. Kweli sekunde kadhaa baadaye, tukakuta basi limepinduka eneo lile lile Roho Mtakatifu alilonionesha. Sasa nikamuuliza Roho Mtakatifu ana maana gani kunionesha ajali ile ilyokwishatokea, kwa nini asinioneshe kabla haijatokea; akaniambia, "kuna mtu alipaswa kuomba kuzuia ajali hii, hakuomba." Nilijiuliza njia nzima sasa Roho Mtakatifu ananieleza hilo mimi nifanye nini, je niombe? Lakini niombee nini? Baadaye Roho Mtakatifu akanisaidia kwa kuniuliza, je wewe si mwalimu? Nikamjibu; akaniambia, unauliza nini, ina maana umesahau wajibu wako? Nikaelewa maana yake nini, nikakaa kimya.
Nia ya kukupa mifano hii ni kutaka tu uelewe kwamba kuna wizara nyingi sana katika kanisa la Kristo zinahitaji watu (maana yake kuna employment opportunities), halafu upo na unadai eti huna cha kufanya unasubiri kwenda mbinguni, pole!
Paulo anasema, mtenda kazi astahiri ujira wake. Mimi nakwambia ukiwajibika, kuna mambo mengine hutamwomba Mungu kama mtoto wake, ila kama mtenda kazi. Sasa kawaulize wafanya kazi ikifika mwisho wa mwezi wakidai mishahara yao wakanyimwa huwa wanafanya nini. Kwa hiyo kuna maeneo mengine na wakati mwingine utamwendea Mungu na kumwambia kumbuka kazi niliyofanya, nakwambia Mungu atajibu hayo maombi mara moja.
Kuna wakati fulani nikiwa Tanga, nilikuwa nina maombi ya watu kiasi kwamba nakosa muda wa kuombea mambo yangu binafsi. Yaani, ukifika muda wa maombi, naomba kwa ajili ya mahitaji ya watu, na kwa jinsi yalivyo mengi nikifikia wakati wa kuombea yangu najikuta naparazaparaza tu na kuondoka. Ikafika wakati nikamwambia Mungu, kuna vitu vyangu sitakuwa naombea; kwa mfano, kuombea chakula, safari zangu n.k. Nikamwambia Mungu kwa wakati nilionao sina muda wa kuombea hivyo vitu, hivyo nikila wewe takasa hicho chakula, nikisafiri tangulia hiyo safari! Kweli Mungu alikuwa mwaminifu kwani alifanya hivyo, kuna wakati nikianza tu kula anasisitiza, usile hicho chakula kitakuumiza, tafuta kingine. Wakati mwingine napanga safari, ghafla anasema usiende hiyo safari. Kumbuka kwamba nikipanga safari ama nikila hata siombi, lakini anasimamia yote. Lakini kitu gani anatazama hapa? Uwajibikaji wangu katika hilo eneo. Sasa usije ukajaribu ukifikiri ni rahisi, hayo yalikuwa makubaliano yangu na Mungu. Kitu ninachotaka uone hapa ni jinsi gani unaweza kusimama mbele za Mungu. Unaweza kusimama kama mwana, ukapata haki za kuwa mwana, lakini pia ukaenda kama mtenda kazi pamoja na Kristo, ukapata ujira. Jina la Mungu libarikiwe!
Wakati fulani nikiwa Tanga Tec nilikuwa na huduma katika shule fulani, na niliahidi kwenda. Siku ile imefika na saa ya kwenda imefika; ghafla, ndani nikasikia wito wa kutokwenda! Haikuwa rahisi kukubali, nikabishana na Roho Mtakatifu kwa kumueleza umuhimu wangu kwenda huko, lakini akaniambia; kwani si uliniambia nisimamie safari zako? Ikabidi nikubaliane naye, nikaahirisha. Baadaye nikapigiwa simu na wale wapendwa kwamba siku hiyo kipindi cha dini kiliingiliwa na ratiba za shule, hivyo hakikuwepo! Ndipo nikaelewa kwa nini Roho Mtakatifu alinizuia kwenda.
Hivyo utumishi ama kutumika kwako ama kutimiza wajibu wako ni muhimu sana katika kupokea haki zako kutoka kwa Mungu. Unaweza Ukasema, nitasimama kama tu mwana na nitapewa hivyo vya kuwa mwana. Lakini nikukumbushe kwamba, mtoto anayejituma sana nyumbani, kwa siku za leo; ndiye baba anamfikiria sana na kumshirikisha katika mambo mengi, na saa nyingine kumuachia urithi pamoja na kwamba mzaliwa wa kwanza yupo. Mara nyingi utamkuta baba yupo naye, akimwelekeza mambo mbalimbali, saa nyingine hata kumuomba ushauri. Sasa wewe kaa kama mtoto goi goi uone, utakuwa mzigo kwa mama yako! (Mwana mwenye hekima ni furaha kwa babaye, lakini mwana mpumbavu ni mzigo kwa mamaye)
Naomba niishie hapa kwa leo, lakini najua utakuwa na maswali; kwa mfano, wewe hujawajibika, na uko katika hali ngumu na unataka Mungu ajibu maombi, akusaidie; ufanyeje? Nitakuletea mfululizo wa pili wenye kicha cha habari TOFAUTI KATI YA NEEMA NA HAKI. Pia katika somo ama mfululizo huo nitakueleza jinsi imani inavyoweza kusimama sehemu ya wajibu, yaani kuvuta haki yako kutoka kwa Mungu kwa kutumia Imani. Pia kama una jambo unataka kuombewa unaweza kututumia kwa e-mail hii, partnersprayer@yahoo.com Wapo watumishi wa Mungu waliopakwa mafuta kuchukua mizigo ya wengine kwa kuwaombea.
Mungu ninayemtumikia akutie nguvu katika hayo yote, zaidi sana kuelewa makusudi yake kwako.
Ni mimi mtumishi wako;
Ev. Azgard S. Chamulungwana
sheghwede@yahoo.com
+255713990607.

JENGO LA KANISA TAG CITY HARVEST LAWEKWA WAKFU RASMI

HATIMAYE jengo Kanisa la TAG City Harvest limezinduliwa na kuwekwa wakfu na Askofu Mkuu wa Tanzania Assemblies of God, Rev. Dk. Barnabas Mt...