Thursday, March 29, 2018

JENGO LA KANISA TAG CITY HARVEST LAWEKWA WAKFU RASMI

HATIMAYE jengo Kanisa la TAG City Harvest limezinduliwa na kuwekwa wakfu na Askofu Mkuu wa Tanzania Assemblies of God, Rev. Dk. Barnabas Mtokambali jumamosi ya wiki iliyopita.

Askofu Mtokambali alisisitiza juu ya sifa za nyumba ya Bwana ambazo ni Utakatifu, Maombi, Uponyaji, Sifa (Mahali pa Kusifu) na Kushinda Vikwazo; akihubiri kutoka kitabu cha Mathayo 21:12-17.

Uzinduzi huo wa City Harvest uliambatana na maadhimisho ya kutimiza miaka saba ya tangu lianze kutoa huduma za kiroho katika jiji la Dar es Salaam.

Tangu Februari, mwaka 2011, Kanisa la City Harvest limeendelea kukua na kupanua wigo katika kutimiza malengo yake hasa kuwasaidia wanataaluma vijana na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.

Muasisi wa City Harvest, Mchungaji Kiongozi, Architect Yared Dondo alipata maono ya kuanzisha kanisa hilo kwa lengo la kuwasaidia vijana wa vyuo kupata uelewa kuhusu masuala ya kiroho na kitaaluma na kuwafikia wanataaluma wenzao kwa Injili ya Kristo.
Mchungaji Dondo ambaye ni Msanifu wa Majengo (Architect) alipata maono hayo wakati akisimamia mradi wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) miaka ya 2007/8.

Katika kipindi hicho, Mchungaji Dondo alishuhudia vijana wengi waliokuwa wanawasili katika eneo la chuo hicho kwa mara ya kwanza, ili kuanza masomo, lakini hapakuwepo na eneo maalum la kuwasaidia vijana kukusanyika kwa ajili masuala ya kiroho kama kuabudu na kumsifu Mungu.
“Niliwaangalia wanafunzi wale wanaingia na mizigo yao wakiwa na nyuso zilizojaa matumaini ya kuanza maisha mapya, kuvumbua mambo mapya na kupata taaluma na bila shaka maisha bora,”
“Moyo wangu uliugua, niliwaza jinsi ambavyo maisha ya Chuo bila Yesu yana mashaka mengi sana. Nikaona jinsi ambavyo rasilimali hii muhimu kwa wazazi na taifa  imepotea bila Yesu,” anaelezea mchungaji Dondo. 

Historia ya City Harvest
City Harvest lilianzishwa Februari 20, 2011, katika ukumbi wa sinema uliopo Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Akielezea changamoto walizozipata pindi wanaanzisha kanisa hilo, Mchungaji Dondo anasema katika kipindi hicho kulitokea changamoto ya aina yake kwani awali walipata ukumbi kwenye jengo lingine, lakini baadae walipata taarifa kutoka kwa uongozi kuwa, jengo hilo haliwezi kutumika katika masuala ya kidini, ikiwa ni siku mbili kabla ya ibada ya kwanza kabisa kufanyika.

“Ilikuwa changamoto kubwa, kwa sababu maandalizi yote yalikuwa yamekamilika, lakini Mungu alituwezesha kupata ukumbi huu wa sinema ingawa gharama ilikuwa kubwa, tukaona tufanye angalau ufunguzi na mambo mengine yatafuata,” anasema.

“Kitu ambacho sitaweza kusahau katika maisha yangu, ni siku ambayo ukumbi wa watu 250 ulijaa na watu wakakaa mpaka kwenye ngazi (steps), wakiwemo watoto wengi; pamoja na kuwa tulibadili sehemu ya kukutania muda wa mwisho”

Kwa kipindi cha wiki 70, sawa na mwaka moja na nusu, City Harvest ilikuwa inalipa kiasi cha Tsh 900,000/- kwa saa tatu kila Jumapili kwenye ukumbi huo wa sinema.

Mchungaji Dondo anasema gharama ya kukodi ukumbi ilikuwa kubwa kumudu lakini sadaka ya Jumapili ya ufunguzi katika ukumbi wa sinema ilitosha kulipa gharama za pango siku hiyo na jumapili iliyofuata. Tulimshangaa Mungu

“Mungu aliendelea kutushangaza hivyo hivyo kwa muda wa miezi 18  hatukupungukiwa,” anasema.

Baada ya hapo mwaka 2012, mtumishi wa Mungu alitupatia ukumbi wa ibada na ofisi Mabibo Gereji, barabara ya Mandela, juu ya jengo la kituo cha Mafuta cha bure.

Hata hivyo, baada ya muda wa miaka 3, tulipokea barua na mamlaka za nchi zinazoshughulika na mambo ya mazingira.  “Barua ilitaka tuondoe kanisa katika maeneo ya biashara yake ya uuzaji mafuta vinginevyo asingeweza kupewa leseni kamili ya biashara yake mahali pale kwa misingi ya kiusalama na athari zinazoweza kutokana na moto”. Mwanzo tulishtuka, lakini tuliikubali changamoto ile.

Hatimaye mwishoni mwa mwaka 2013, tulianza maandalizi  kisaikolojia na maombi  kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa.  Mchungaji Dondo aliunda kamati ya ujenzi Januari 2014 ambapo baadae Mungu alitusaidia kupata fremu ya jengo la kanisa (Prefabricated structure) kutoka Marekani.

Kutokana na walengwa wa huduma yetu kuwa wanafunzi hasa wa vyuo vikuu tulitafuta sana viwanja na kanisa viwe karibu na wanafunzi. 

“Tulitembelea viwanja vingi maeneo hayo na gharama zilikuwa kubwa, vingi pia vilikuwa vidogo lakini bei kubwa, tuliendelea tulimuamini Mungu kutupatia kilicho bora machoni pake”.  

Baadaye, aliyekuwa Askofu wa Mkuu wa TAG, Rev. Dk. Ranwell Mwenisongole ambaye ni Mchungaji Kiongozi wa kanisa la TAG CCC - Upanga alituwezesha kupata kiwanja hiki cha Bahari Beach ambapo sasa jengo limejengwa.

Usanifu wa Jengo la City Harvest
Kiwanja cha City Harvest kina kubwa wa mita za mraba 8,000 na jengo hilo lina ukumbi wa ibada wa kukaa watu zaidi ya 1,000, vyumba vya madarasa vitano na ofisi za wachungaji. 

Nje ya jengo kuna nyumba kwa ajili ya umisheni (Missions House) ambayo inatumika kwa ajili ya maandalizi ya kwenda missions au ushuhudiaji au kufanya kambi za maombi.

Pia eneo lingine limetengwa kwa ajili kiwanja cha michezo ambacho kwa sasa kipo wazi kwa ajili ya watoto wote.  Aidha huko mbeleni tuna mpango wa kujenga shule ya awali (Nursery School) ya kimataifa ambayo tayari iko kwenye matumizi ya mpango miji (land use plan).

City Harvest mpaka sasa ina wachungaji wapatao 15.  Kati yao wapo wachungaji wanaotumika kanisani muda wote na wengine ni wachungaji washiriki (Associate Pastors). 

Kanisa la Kimisheni
City Harvest ni kanisa la kimisheni, kwa miaka saba tumepeleka timu za umisheni South Sudan, Msumbiji, Kigoma, Rufiji, Mkuranga, Bagamoyo, Lindi, Tandahimba, Kibaha (Bonde la Baraka), Moshi na AfriKa ya Kusini.

Pia mwaka jana kwa kushirikiana na jimbo la Dodoma Kusini (Mpwapwa) kanisa hilo lilifanikiwa kupanda makanisa manne   Winza, Chogola, Chipogoro na Mtera katika mkoa wa Dodoma ikiwemo kununua kununua viwanja vine, kujenga jingo la Kanisa moja na kutegemeza wachungaji saba kwa sasa.  Tumeweza kununua kiwanja cha kanisa Lindi mjini na tunao mpango wa kufungua kanisa India, ili kuwafikia wanafunzi wa vyuo wa kitanzania wanaosoma huko. Tayari tumeshapata jengo Bangalore.

Mipango ya kanisa mwaka huu ni kupanda makanisa mengine manne huko (Mpwapwa), kwa kuanzia kulingana na mpango kazi aliotupa Askofu Mkuu. Kupitia kazi hii, Mungu ameibua vipawa mbalimbali katika kanisa kama wainjilisti, waalimu na hata uzoefu wa ushuhudiaji, na mwili wa Kristo umejengwa. Tunamtukuza Mungu. Pia tumefungua tawi la kanisa kule Kigamboni ili kuwafikia wanavyuo wanaokaa maeneo hayo na pia, tumeanzisha Bible Study, Haidary Plaza, ghorofa ya pili, kila Alhamisa saa 11.30 jioni, kuwasaidia kujifunza maandiko wanaofanya kazi katikati ya jiji na maeneo ya Posta.

Changamoto
Changamoto kubwa ya kanisa inatokana na maono ya kanisa kuwa wanafunzi ni washirika wa majira na nyakati. “Vyuo vikifunguliwa wanapatikana, vikifungwa wengi wanaondoka.  Hivyo tunakuwa na muda mfupi wa kuwahudumia pia wanapohitimu wanasambaa kutafuta ajira” 

Pia Kanisa linahitaji vifaa vya umisheni kwa ajili ya huduma za mikoani ambazo zinatawezesha kuwafikia watu wengi kiurahisi.

Kanisa la City Harvest linamshukuru Mungu kwa kufafanikisha kumalizia kazi ya ujenzi na mambo yate makubwa ambayo yameonekana kipindi chote.

“Mungu ni mwema sana, hadi sasa hatuna deni wala hatudaiwi na mtu au taasisi yoyote, Tumefanikiwa kuwa huru kwa madeni”, anasimulia Mchungaji Dondo.

Kanisa la City Harvest lilopo Bahari Beach pia limeanzisha huduma zinazoendelea kila Alhamisi saa 11 jioni katikati ya jiji kwenye jengo la Haidery Plaza na pia katika Kigamboni kila jumapili kuanzia saa 10 alasiri eneo la Boat Beach, Maweni Mbuyuni.

Kwa mawasiliano na kanisa la City Harvest, kwa maombi, maombezi na mengineyo, piga simu namba 0654320122 au tembelea ukurasa wa Facebook kujionea habari, picha, video na mafundisho kwa kutafuta jina la City Harvest Church Dar es Salaam. Waweza pia kuandika barua pepe kupitia anuani ya: cityharvestdar@yahoo.com

Thursday, March 22, 2018

UZINDUZI WA JENGO LA KANISA, TAG CITY HARVEST BAHARI BEACH JUMAMOSI HII. USIKOSE!

Kanisa la TAG CIty Harvest linakukaribisha kwenye uzinduzi wa jengo lake la kanisa lilopo Bahari Beach na Mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Kanisa la TAG Tanzania, Askofu Barnabas Mtokambali

JENGO LA KANISA TAG CITY HARVEST LAWEKWA WAKFU RASMI

HATIMAYE jengo Kanisa la TAG City Harvest limezinduliwa na kuwekwa wakfu na Askofu Mkuu wa Tanzania Assemblies of God, Rev. Dk. Barnabas Mt...